Watu 11 wakamatwa kwa kusambaza taarifa za uzushi kuhusu Rais Samia

0
46

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 11 kwa makosa ya kusambaza taarifa za uongo na uzushi zinazomhusu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali kupitia akaunti za mitandao ya kijamii.

Akizungumza Kamanda wa Polisi, Jumanne Muliro amesema kwa kushirikiana na timu maalum ya kuzuia na kupambana na makosa ya mtandao ilifanikiwa kuwakamata watu hao akiwemo Alex Magoti (26) mkazi wa Tabora na wenzake wanne kwa tuhuma za kumiliki runinga za mtandaoni na akaunti za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa hizo.

Amesema watu hao wamekuwa wakiweka taarifa za upotoshaji mtandaoni zinazotambulika kwa majina ya BSUN Online TV, Gattu Online TV, Tamutamu online TV, Kilimanjaro online TV.

Amuua mkewe baada ya kuambiwa mtoto si wake

“Mfano wa taarifa hizo ni ‘Rais Samia akosoa vikali utawala wa JPM, aanika ukatili aliofanya, Imevuja video, Mbowe apewa shavu, Deni la taifa laibua mazito Mwigulu kutumbuliwa, Ghafla mke wa Magufuli afa, na Itakutoa machozi ukweli wote kifo cha Magufuli,” amesema.

Aidha, Kamanda Muliro amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni Li Naiyong (48) raia wa China ambaye alijihusisha na shughuli za kuingilia mfumo wa mawasiliano kinyume cha taratibu za nchi na kuisababishia Serikali hasara ya TZS milioni 221.16.

Kamanda Muliro ametoa rai kwa wananchi kuwa makini na mitandao ya kijamii pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazoepuka kuchapisha taarifa za uongo na kuleta taharuki kwa wananchi.