
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Iinawashikilia watu 12 wanaodaiwa kuwa wahalifu, wakiwa wamejificha kwenye mapango mbalimbali yaliyomo mkoani humo, huku wakidaiwa kuwa na vifurushi vya bangi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema operesheni hiyo ni baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu wahalifu wanaojificha katika mapango na maeneo ya milimani wakijiandaa kufanya matukio ya uhalifu, hasa kuelekea mwishoni mwa mwaka.
Kamanda Mutafungwa amesema operesheni hiyo iliyoanza rasmi Novemba 29, 2025 ilifanyika katika mapango mbalimbali yaliyopo katika Wilaya ya Ilemela na Wilaya ya Nyamagana ikihusisha maeneo ya Kata za Isamilo, Ibungilo, Mkolani, Mhandu, Igoma Kati, Buhongwa, Kitangili, Bwiru na Kawekamo.
Aidha, Kamanda ameeleza kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kufanyiwa mahojiano ili taratibu nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa, huku akitoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya kihalifu.








