Watu 19 wauawa nchini Afrika Kusini

0
19

Takriban watu 15 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye sialaha katika baa moja iliyopo kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini siku ya Jumapili Julai 10, mwaka huu.

Polisi wamesema kundi la vijana lenye bunduki na bastola walishambulia eneo hilo kwa kufyatua risasi ovyo kisha kutoweka na kwamba mpaka sasa bado hawajatambua chanzo cha tukio hilo.

Taarifa zinasema waathirika wa mauaji hayo wanadaiwa kuwa na umri kati ya miaka 19 na 35, huku wengi zaidi wakijeruhiwa vibaya na sasa wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

“Miili ilikuwa juu ya kila mmoja huku damu zikiwa zimetapakaa. Tulikuwa tunawatafuta wapendwa wetu, ikabidi turuke miili kuwatafuta ndugu zetu,” amesema mkazi wa eneo hilo.

Aidha, Mkuu wa Polisi wa Jimbo la Gauteng, Luteni -Jenerali Elias Mawela, amesema ufyatuaji risasi huo unaonekana kuwa shambulio la kinyama dhidi ya watu wasio na hatia wa Tavern.

Katika tukio lingine, polisi wameripoti vifo vya watu wengine wanne waliouawa katika shambulizi tofauti katika mkoa wa Kusini-Mashariki mwa KwaZulu-Natal usiku wa Jumamosi.

Polisi wamesema wanaendelea kuwasaka washukiwa hao ambao bado hawajafahamika majina yao mpaka sasa.

Rais Cyril Ramaphosa ametoa salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa waathiriwa wa visa vyote viwili na kulaani matukio hayo ya kinyama.

“Kama taifa, hatuwezi kuruhusu wahalifu wa kikatili kututisha kwa njia hii, bila kujali ni wapi matukio kama haya yanaweza kutokea,” amesema.

Send this to a friend