
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watu 39 kwa tuhuma za kufanya fujo na kusababisha usumbufu kwa jamii katika maeneo ya Bububu, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Tukio hilo limetokea Julai 28, 2025, saa 12:30 jioni, ambapo kundi hilo linalodhaniwa kuwa ni sehemu ya mkusanyiko maarufu unaofahamika kama “Kanga Moja” lilikuwa likitokea maeneo ya Kiwengwa (Kaskazini Unguja) na Michungwa Miwili (Magharibi A), wakiwa kwenye msafara wa magari, pikipiki, na vyombo vingine vya moto.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, msafara huo ulikuwa ukicheza muziki kwa sauti ya juu barabarani, huku baadhi ya washiriki, wanaume na wanawake, wakidaiwa kufanya vitendo vya kuudhi jamii.
“Watuhumiwa hao, wanawake 24 na wanaume 15, walikuwa wakicheza mitaani wakiwa kwenye magari huku baadhi yao wakionesha maungo yao wazi, jambo ambalo liliwashtua na kuwakera wakazi wa maeneo waliyopita,” imesema taarifa ya Polisi.
Aidha, magari matatu yametiwa mbaroni, ikiwemo Town Ace mbili zenye namba za usajili Z 403 YJ na Z 784 LL, zote zikiwa zimefungwa spika kubwa pamoja na basi aina ya Coster lenye namba za usajili Z 306 lililokuwa limewabeba zaidi ya abiria 27.
Kwa sasa, watuhumiwa wote wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika.








