Watu 4,060 wamefariki kwa ajali za barabarani nchini tangu mwaka 2020

0
40

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi Desemba mwaka 2022 jumla ya ajali zilizotokea barabarani nchini ni 5,132 ambazo zilichukua maisha ya watu 4,060 na kusababisha majeruhi na walemavu 6,427.

Ameyasema hayo wakati akishiriki Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika mkoani Mwanza Machi 14, 2023 ambapo amebainisha kuwa jumla ya abiria 1,582 walifariki katika ajali mbalimbali huku  abiria 4,372 wakijeruhiwa, na jumla ya madereva 509 walipoteza maisha na madereva 584 kujeruhiwa.

Mambo yatakayojadiliwa Makamu wa Rais wa Marekani akitembelea Tanzania 

Kwa upande wa watembea kwa miguu waliopitiwa na vyombo vya usafiri barabarani na kupoteza maisha ni 959 na watu 650 walijeruhiwa huku wapanda pikipiki 797 walifariki na 725 walijeruhiwa, na wapanda baiskeli 196 walipoteza maisha  na wengine 82 walijeruhiwa.

Aidha, Waziri Mkuu amelielekeza Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuhakikisha mabasi ya abiria yanayokwenda umbali mrefu yanakuwa na madereva zaidi ya mmoja ili kuepusha ajali zinazotokea.

“Mabasi hususani yanayoenda mikoani yale ya safari ndefu [..] ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani. kwanini? Hatukufuata zile kanuni za waendesha mabasi haya ya umbali mrefu kuwa asiendeshe mtu mmoja, lazima kuwe na madereva kuanzia wawili na kuendelea, ili wapeane nafasi ya kuendesha anapumzika,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Send this to a friend