Watu sita wafariki ajalini mkoani Arusha wakitokea msibani

0
16

Watu sita wamefariki dunia na wengine sita wamejeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari dogo aina ya Land Cruiser hardtop na Lori eneo la Kambi ya Jeshi Sofa mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni amethibitisha kutokea kwa ajili hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika Barabara ya Arusha – Dodoma, wilayani Monduli.

Hamduni amesema gari dogo mali ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu Parokia ya Masakta Babati liligonga tela la lori hilo lililokuwa limesimama baada ya kupata hitilafu ya kiufundi.

Wote waliofariki (wanaume 5 na mwanamke 1) walikuwa kwenye Land Cruiser na walikuwa wakirejea Babati kutoka msibani wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Mwili wa mtu mmoja umetambuliwa kwa jina la Father Sixtus S/O Massawe, umri kati ya miaka 55-60, Paroko wa Parokia ya Masakta Babati na miili mingine bado haijatambuliwa.

Polisi wameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Land Cruiser ambaye alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi pasipo kuchukua tahadhari ya uendeshaji wakati wa usiku wa kupelekea ajali hiyo.

Majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa matibabu, miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ua Wilaya ya Monduli kwa uchunguzi wa daktari.

Send this to a friend