Watu sita wakamatwa kwa kuhujumu miundombinu ya reli ya SGR

0
8

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watuhumiwa wawili, Said Sempinga (39) na Michael Robert (44) wote wakazi wa Kilosa kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli ya mwendokasi ya SGR.

Tukio hilo limetokea Oktoba 03, mwaka huu majira ya saa 05 usiku katika kijiji cha Msagali, Wilaya ya Mpwapwa mkoani humo, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kukata na kuiba waya wa shaba (copper wire) kutoka katika madaraja matatu ya reli hiyo.

“Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kuanza uchunguzi wa tukio hilo mara moja kwa kushirikiana na wananchi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti wakiwa na hizo nyaya za shaba walizoiba kwenye reli ya umeme ya mwendokasi SGR,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wanne kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kuharibu na kuiba miundombinu ya Serikali kwa kukata nyaya za shaba katika mradi wa treni ya umeme SGR wilaya ya Bahi.

Watuhumiwa hao ni Said Kapambwe (38), Petro Reng’aisi (22), Michael Leyaseki (27) na Issa Misami (42) ambapo watuhumiwa hao tayari wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Dodoma.

Send this to a friend