
Jeshi la Polisi linawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya Castory Casian Madembwe, mtumishi wa TAASAF na mkazi wa Ipuli mkoani Tabora.
Tukio hilo lilitokea Juni 10, 2025 eneo la Ipuli, Tabora ambapo baada ya mauaji hayo watuhumiwa hao wanadaiwa kuufukia mwili huo nyuma ya nyumba aliyopanga mmoja wa watuhumiwa hao na kisha kupanda nyanya juu yake.
Watuhumiwa hao ni Nelson Samweli, mkazi wa Ipuli Tabora (mpangaji wa nyumba ambayo mwili huo ulifukiwa), Salum Heri, mkazi wa Kadinya, Bathoromeo Michael, mkazi wa Isevya, Juma Ramadhan, mkazi wa Kidatu na Mohamed Hamad, mkazi wa Uledi. Mtuhumiwa mwingine ni Careen Matemba, mke wa Nelson Samwel aliyekimbia baada ya kusikia wenzie wamekamatwa.
Jeshi la Polisi limesema walifanikiwa kumkamata Nelson Samwel akiwa na simu ya marehemu na alipohojiwa alikwenda kuonesha walipofukia mwili huo, na ndipo taratibu za kisheria na za kisayansi zilifanyika kuufukua mwili.
“Pamoja na watuhumiwa kumuua Castory Madembwe, bado walimpigia simu mama yake na kumwambia mtoto wako ametekwa, ukitaka tumwachie tuma fedha, na kabla ya kukamatwa watuhumiwa hao, mama huyo alikuwa amekwishawatumia shilingi milioni tano,” imesema taarifa ya Polisi.








