
Mahakama ya Wilaya ya Mvomero imewahukumu vijana wawili kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi Antony Reuben Ngoi katika shauri la jinai namba CC 309/2026, kwa watuhumiwa hao ambao ni Gaudence Simon (25) maarufu kama Mwananchi na Galus Charles (20) maarufu kama Mwimbe, wote wakazi wa kijiji cha Yowe, kata ya Homboza wilayani Mvomero.
Mahakama imethibitisha kuwa Disemba 25, 2025, majira ya saa 11 alfajiri katika pori la Kidugulu, washitakiwa walimvamia mfanyabiashara Dimoso Enias Kibendera (29) na kumjeruhi vibaya kwa kutumia silaha kali kabla ya kumpora fedha taslimu Tsh 400,000, mizigo ya biashara (viatu, malapa, na nguo), simu ya mkononi na mali nyingine zenye thamani ya jumla Tsh 730,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema kufanikishwa kwa kesi hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Polisi wa Kituo cha Mvomero na wananchi, kuanzia hatua za awali za ukamataji hadi ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.








