Wawili wafariki, 58 walazwa baada ya kudaiwa kula chakula chenye sumu kanisani

0
24

Hali ya simanzi imetanda katika Hospitali ya Emuhaya, Kaunti ya Vihiga nchini Kenya, baada ya watu wawili akiwemo mtoto, kufariki dunia kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa ni sumu kwenye chakula kilicholiwa kanisani.

Mkurugenzi wa Afya Kaunti ya Vihiga, Dkt. Benjamin Onduso amesema wagonjwa wawili walifikishwa hospitalini siku ya Jumatatu saa nne asubuhi wakiwa na dalili za kuharisha maji maji na kutapika.

“Wagonjwa hao walipatiwa matibabu na hali yao ikatulia, lakini kuanzia saa tano asubuhi, idadi ya wagonjwa wenye dalili sawa ilianza kuongezeka,” amesema Dkt. Onduso kutoka hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa taarifa, chanzo cha tatizo hilo linahusishwa na chakula aina ya wali na maharagwe kilicholiwa wakati wa harambee iliyofanyika Jumapili katika kanisa la PAG eneo la Luanda.

Zaidi ya waumini 58 wa kanisa hilo wamelazwa hospitalini humo, huku wawili wakiwa katika hali mahututi wakipigania maisha yao.

Dkt. Onduso amesema sampuli za wagonjwa na mabaki ya chakula kinachoshukiwa kuwa na sumu zimesafirishwa kwa uchunguzi zaidi na matokeo yanatarajiwa hivi karibuni.

Send this to a friend