Wawili wakamatwa kifo cha Mwenyekiti wa Vijana CCM
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Machinjioni, Kata ya Bwawani, Michael Kalinga (36) mkazi wa Makongolosi wilayani Chunya.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema Desemba 02, 2024 saa 5 usiku eneo la Mikoroshini, Kalinga alikutwa amefariki na mwili wake kutelekezwa porini umbali wa mita 250 kutoka barabara ya Makongolosi baada ya kupigwa na kitu butu kichwani na watu ambao hawakufahamika kabla, ambao pia walifanikiwa kumpora pikipiki yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.
“Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali ambapo Desemba 03, 2024, huko Mlowo, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe llilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo wakiwa na pikipiki waliyopora kutoka kwa Michael Kalinga. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili hatua nyingine za kisheria zifuatwe,” imeeleza taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja, kwani uhalifu haulipi na badala yake wajihusishe na shughuli halali za kujipatia kipato.