Wawili wauawa baada ya wananchi kuvamia kituo cha polisi 

0
12

Watu wawili wamefariki dunia baada ya wananchi takriban 800 kuvamia na kufanya vurugu katika kituo cha polisi Lulembela wilayani Mbogwe mkoani Geita wakiwashutumu wa wawili kuwa ni wezi wa watoto

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema vurugu hizo zilianzia katika eneo la mnada wa Lulembela baada ya watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba watoto wawili, na wananchi waliokuwa katika mnada huo walihisi kuwa ni wezi wa watoto na kuanza kuwashambuilia, ndipo akatokea Mtendaji wa Kata akawabeba kwenye pikipiki na kuwakimbiza katika kituo cha Polisi Lulembela.

Ameeleza kuwa baada ya watu hao kufikishwa katika kituo cha polisi, wananchi walifika katika kituo hicho na kuwataka askari polisi wawakabidhi watuhumiwa hao ili wawaadhibu, ambapo askari hao walijaribu kuwazuia lakini walikaidi na baada ya askari kuona hali hiyo ya kuhatarisha maisha ya watu na mali za serikali walitumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu hao na iliposhindikana walitumia silaha za moto kwa kupiga risasi juu ili watu hao watawanyike.

Ameongeza kuwa na mbali na kushambulia kituo hicho kwa mawe na kutaka kuingia kwa nguvu ndani ya kituo hicho, wananchi hao walichoma moto gari moja lenye namba za usajili T.440 ATW aina ya Toyota Cardina lililokuwa limeegeshwa nje ya kituo hicho.

“Katika vurugu hizo watu wawili wamepoteza maisha, mmoja ni mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 20 na wa pili ni msichana aitwaye Teresia John mwenye umri wa miaka 18, mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lulembela ambaye nyumba yao inatazamana na kituo hicho cha Polisi.”

“Hata hivyo, ilibainika kuwa watu waliokuwa wamebeba watoto hao ni Emanuel John (33) mkazi wa Kigamboni Lulembela ambaye alikuwa amembeba mtoto wake aitwaye Ikram Emanuel mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja na wa pili anaitwa Ng’amba Leonard (24) ambaye alikuwa amembeba mtoto aitwaye John Emanuel mwenye umri wa miaka miwili na miezi nane. Mama wa watoto hao aitwaye Rachel Masunga Luhende (22) mkazi wa Kigamboni Lulembela amethibitisha kuwa watoto hao ni wa kwake na walikuwa kwa wifi yake ambapo baba yao mzazi na mjomba wao walikwenda kuwachukua,” imeeleza taarifa.

Aidha, imesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea sambamba na ukamataji wa waliohusika katika vurugu hizo.

Send this to a friend