Wazazi wakamatwa wakiwafunza ngono watoto chini ya miaka 8

0
47

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linawashikiliwa wazazi 35 kutoka Kata ya Nalasi waliokuwa wakiwafundisha watoto wa kike wenye umri chini ya miaka nane mbinu za kufanya ngono (maarufu Msondo) na kuishi na wanaume.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amesema wazazi hao wamekamatwa usiku wakiwa wamejifungia kwenye nyumba mmoja baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema.

Mbali na wazazi hao, pia polisi wamewakamata kungwi mmoja, Mtendaji wa Rajabu Lusanga na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nalasi, Ali Omari kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wazazi hao licha ya kuishi jirani na eneo la tukio hilo.

Mtatiro ametoa onyo dhidi ya wazazi wanaoendekeza mafundisho ya Msondo na kuwa msako utaendelea kwani vitendo hivyo vinachangia sana kuongezeka kwa mimba na wasichana wengi kuacha shule.

Baadhi ya wakazi wa Tunduru wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kukomesha mila potofu ambazo zimekuwa chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa watoto wa kike na wengine kuacha masomo.

Send this to a friend