Wazazi warudisha mahari kuwanusuru watoto wao wanaoteseka kwenye ndoa

0
41

Wazazi wawili waliowaoza binti zao wenye umri wa miaka 14 wamekubali kurejesha fedha na mifugo waliyopokea kama mahari na kurudi na watoto wao nyumbani baada ya kugundua kuwa watoto hao wamekuwa wakiteseka kwenye ndoa zao.

Hayo yameelezwa na mtendaji wa kijiji cha Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Selemani Kibakaya baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Woman Wake Up (Wowap).

“Tulikaa kikao cha pamoja baina ya wazazi na tukapitisha maamuzi mahari irudishwe ambayo ilikuwa shilingi 400,000, mbuzi watatu na magunia matatu ya mtama, wazazi wakarudisha mahari na binti yuko kwa wazazi wake,” amesema Kibakaya.

Ameongeza kuwa binti mwingine wa kijiji hicho aliolewa akiwa na miaka 14 akaishi na mwanaume ambaye baadaye alienda mkoani Mbeya kutafuta maisha.

“Wazazi walikiri kufanya makosa kumuoza binti yao, wakakubali kurudisha mahari shilingi 150,000, mbuzi mmoja na gunia mbili za mtama na sasa binti yuko mikononi mwa wazazi wake,” ameongeza.

Naye Mratibu wa Wowap, Nasra Suleiman amesema vitendo vya ukatili kwa watoto vimekithiri katika Mkoa wa Dodoma, na imebainika kuwa vinachangiwa zaidi na uelewa mdogo wa haki za watoto pamoja na hali duni za kimaisha.

Chanzo: Habari Leo

Send this to a friend