Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali la Vuka Initiative, Veronica Ignatus amewahasa wazazi na walezi juu ya kulaza watoto wao na wageni katika nyumba zao kwa kile kilichoelezwa kuwa baadhi yao huwafanyia watoto vitendo vya ukatili.
Amezungumza hayo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, ambayo yalikwenda sambamba na kampeni ya ‘Mlinde mtoto wa kiume’ iliyokuwa na lengo la kuwakumbusha wazazi kuwajengea watoto misingi imara.
“Hakuna kuaminiana, ni kheri uchukiwe na ndugu lakini uponye kizazi chako, hao mnaowaona wema na kuwakaribisha kuwalaza na watoto wenu, wakati mwingine wamekuwa wakiwatishia watoto na wao kuingia woga wa kusema vitendo vya kikatili wanavyotendewa,” amesisitiza Ignatus
Ameongeza kuwa asilimia kubwa ya watoto wanafanyiwa ukatili na ndugu wa karibu waliopo nyumbani, wengi wakiwa ndugu ambao familia zinawaamini na kuwakaribisha.
“Mgeni kama ameweza kujisafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine anakuja kutembelea nyumbani kwako na unafahamu kuwa nyumba yako haina vyumba vya kutosha kumkirimu, kwanini usimtafutie nyumba ya wageni akapumzike huko hadi siku atakavyoona vyema kuondoka?” amesema.
Naye Inspekta Happy Mshana kutoka Dawati la Jinsia Mkoa wa Arusha, amewaonya wazazi dhidi ya tabia ya kupoteza ushahidi wa kesi kwa kutetea uovu kwa kigezo cha kutaka kulinda hadhi ya familia.