Wazazi watakaoshindwa kuandikisha watoto shule kushitakiwa mahakamani

0
22

 

Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema kwamba wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule wakati shule zitakapofunguliwa Januari 17 mwaka huu watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Waziri Ummy amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya kufunguliwa kwa shule.

Amesema kwamba kuzaa mtoto ni jukumu la mzazi na mtoto huyo kupata elimu ni jukumu la serikali, hivyo itahakikisha kila mtoto mwenye sifa za kupata elimu anapata haki hiyo.

“Alisema Waziri Mkuu, mtoto ni wa kwako, haki yako umemzaa lakini wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni tutawachukulia hatua kali ikwemo kuwapeleka mahakamani,” ameeleza.

Waziri ameendelea kusisitiza kupunguzwa kwa vikwazo ambavyo vinaweza kusababisha watoto kushindwa kwenda shule ikiwemo michango ambayo amesema mtoto anatakiwa kuchangia akiwa tayari ameandikishwa shule, na sio kuzuiwa kuandikishwa kwa sababu ya mchango.

“Hatutaki vikwazo kwa wanafunzi wetu. Tunataka watoto wetu wawe darasani tarehe 17,” amesisitiza waziri Ummy.

Kuhusu michango amesema kwamba kama kuna mchango wowote unaotakiwa kutolewa utafuata utaratibu na kibali kitatolewa na mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa.

Serikali ya Tanzania inatoa TZS bilioni 26 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila ada, fedha ambazo zinatarajiwa kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi.

Send this to a friend