Katika tukio la kushangaza lililotokea katika kijiji cha Kiamachongo, Bobasi nchini Kenya, wazazi wazee wameamua kubomoa nyumba ya mtoto wao mmoja kufuatia mzozo wa ardhi uliosababisha mgawanyiko mkubwa katika familia yao.
Mzee Arati Momanyi na mkewe wamechukua hatua hiyo ya kuvunja nyumba ya mtoto wao baada ya kudaiwa kutishiwa na mtoto huyo ambaye pia aliwatuhumu kuwa wachawi.
Akizungumza kiongozi wa eneo hilo, Dickson Omaywa ameeleza kuwa kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya Mzee Momanyi na watoto wake kuhusu mipaka ya ardhi na kusababisha hali ya kutoelewana na kutokuwa na usalama katika boma hilo.
Mzee Momanyi, kwa huzuni, ameeleza kuwa watoto wake watatu wamegeuka dhidi yake na sasa wanataka kumuua ili warithi kipande chake cha ardhi. “Watoto wangu wengine wawili wako upande wangu,” ameongeza.
“Ninauliza serikali, je, hili ni sawa kweli? Je, mtu anapozeeka inamaanisha kuwa ni mchawi? Kwa nini wamegeuka dhidi yangu na mama yao? Kwa nini wanataka kunifukuza kwenye ardhi yangu?” amrhoji Mzee Momanyi huku akionyesha wasiwasi wake juu ya usalama wake na mkewe.