Waziri aagiza kumbi za starehe, MCs, wasajiliwe kabla ya Novemba 30

0
48

Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro ameagiza wamiliki wa kumbi zote za starehe nchini kuhakikisha wanasajili kumbi hizo kabla ya Novemba 30 mwaka huu.

Ameyasema hayo wakati alipolitembelea Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ambapo amefafanua kuwa usajili unaofanyika unalenga kusaidia kutambua ubora na usalama wa kumbi hizo, maeneo yalipo na kuhakikisha kuwa zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

“Natoa rai kwa wananchi wote, popote walipo ambao wanamiliki hizo kumbi kuhakikisha wanazisajili kabla ya Novemba 30, 2023. Baada ya tarehe 30, Novemba tutafanya ukaguzi na yule ambaye tutamkuta hajasajili kumbi zake kwanza atalipa ada ya usajili, lakini pili atatozwa faini kwa mujibu wa kanuni zilizopo,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Aidha, amewaagiza maafisa Utamaduni wa Halmashauri zote kuhakikisha ifikapo tarehe hiyo tayari wawe wamewasilisha taarifa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo pamoja na BASATA kuhusiana na usajili wa kumbi za starehe, usajili wa wasanii pamoja na usajili wa washereheshaji (MCs) ili kila Mtanzania awekwe rasmi katika kila fani yake, na kukuza sekta ya sanaa nchini.

Send this to a friend