Waziri aagiza Simba iandikiwe barua viti vilivyong’olewa vilipwe

0
40

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwaandikia barua Simba SC juu ya ung’olewaji wa viti uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mchezo wa Kimataifa wa Kombe la Shirikisho dhidi ya CS SFAXIEN.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa Wizara hiyo, imeiagiza klabu ya Simba kuwanakiri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu huo zilipwe.

“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubaliki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja na kuwaandikia Simba Sports Club na TFF, wapeni ushirikiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe,” amesema Profesa Kabudi.

Aidha, Waziri Kabudi amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.

Kutokana na uharibifu huo, taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imesema itashirikiana na mamlaka zingine kuwachukulia hatua wote waliohusika katika vurugu hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya refa wa mchezo huo kuchezesha mechi zaidi ya dakika saba zilizoongezwa jambo lililopelekea Simba SC kupata goli la pili la ushindi, na ndipo mashabiki, wachezaji na bench la ufundi la timu ya CS SFAXIEN kufanya vurugu.

Send this to a friend