Waziri afuta likizo za Krismasi na Mwaka Mpya, aagiza mradi ukamilike kwa wakati

0
38

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesitisha likizo za sikukuu za Krimasi na mwaka mpya kwa wataalamu wote wanaohusika na ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo leo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambapo ameagiza wataalamu wote kuwa hapo wakati wote na waendelee na shughuli za ujenzi.

“… hakuna Krismasi, hakuna mwaka mpya, hakuna Jumamosi na Jumapili, hakuna mvua na jua kwenye mradi huu. Wataalamu wote wawepo saa 24,” amesisitiza Kalemani.

Aidha, amewataka wale wote wanaotoka nje ya nchi ambao wangependa kwenda kujumuika na familia zao, wawaambie wanafamilia wao wawafuate kwenye mradi huo wajumuike huko kwani umuhimu ni kuwa na familia na si kusafiri.

Wakati huo huo ameagiza wataalamu zaidi ya 20 ambao walitakiwa kuwepo kwenye mradi huo lakini hajawakuta, wawe wamefika eneo la kazi ifikapo Disemba 31 mwaka huu.

Mradi huo unaojengwa na mkandarasi ambaye ni JV Arab Contractors kutoka nchini Misri utazalisha umeme megawati 2115 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2022.

Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji kati ya Serikali ya Tanzania na Misri ulifanyika tarehe Disemba 12, 2018 na mkandarasi alikabidhiwa rasmi eneo la mradi, Februari 14, 2019.

Send this to a friend