Waziri asema hali ya usalama mpaka wa Tanzania na Msumbiji haitabiriki

0
34

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema hali ya usalama katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji ni ya wastani na isiyotabirika kutokana na uwepo wa kundi la kigaidi la Ansar Al Sunna Wal Jammah (AASWJ) lililoweka kambi Kaskazini mwa Msumbiji mkabala na mkoa wa Mtwara.

Akizungumza bungeni jijjini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa kundi hilo limeweka ngome katika Wilaya ya Macomia mkoa wa Cabo Delgado nchini humo ambapo limeendelea kuhatarisha amani na usalama katika eneo hilo.

“Limebuni mbinu isiyotumia nguvu (Non – Violence Radicalization) ya kuwafikia washirika wapya kwa njia ya amani. Vilevile, limeendelea kujiimarisha kwa kupata wafuasi na silaha kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo kwa kupora kutoka vikundi vya ulinzi na usalama nchini Msumbiji,” ameeleza Waziri Bashungwa.

Aidha, amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa kukabiliana na hali hiyo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji kwenye nyanja za mafunzo, kubadilishana taarifa na kufanya operesheni za kijeshi za pamoja.

Send this to a friend