
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe ametoa muda siku nne huduma ya mabasi ya mwendokasi irejee katika maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Prof. Shemdoe ametoa agizo hilo leo wakati akizindua safari za mabasi ya mwendokasi kutoka kituo cha Ubungo Maji hadi Gerezani. Huduma hiyo ilikuwa imesimama tangu Oktoba 29, 2025 kutokana na vurugu na uharibifu wa baadhi ya vituo.
Uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyeelekeza huduma hiyo irejeshwe ndani ya siku 10. Kwa mujibu wa Prof. Shemdoe, hatua hiyo imekamilishwa ndani ya siku sita tu.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu alituelekeza ndani ya siku 10 tuwe tumekamilisha marekebisho ya muda kutoka hapa Gerezani hadi Kimara, leo nina furaha kusema kwamba ndani ya siku sita tumeweza kusogeza huduma hii hadi Ubungo Maji,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa maeneo mengine kama Kimara, Magomeni na Morocco bado yanaendelea kufanyiwa ukarabati kwa ushirikiano kati ya DART, UDART, TANESCO na TANROADS. Pia amesisitiza kuwa huduma kamili inapaswa kurejea ndani ya siku nne zijazo kama alivyoelekeza.








