Waziri Bashe aagiza Diwani wa CCM ashikiliwe kwa tuhuma za ubadhirifu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa agizo la kushikiliwa kwa diwani wa Chiwale (CCM), wilayani Masasi, Yusuph Mataula ili kusaidia uchunguzi katika sakata la ubadhirifu wa shilingi milioni 139.
Waziri Bashe ametoa maagizo hayo wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Chiwale wilayani Masasi, Mtwara, baada ya kusikiliza kero mbalimbali zinazoathiri maendeleo ya kilimo katika kijiji hicho.
Katika mkutano huo, Bashe alifahamishwa kuwa baadhi ya wakulima wa korosho amba oni wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nanyindwa AMCOS hawakulipwa kiasi cha shilingi milioni 139 katika msimu wa 2016/17 hatua iliyosababisha mali za AMCOS hiyo ikiwemo trekta na lori kupigwa mnada kwa amri ya mahakama.
Mmoja wa wanachama ameeleza kuwa katika kulipatia ufumbuzi suala hilo, uongozi mpya wa Nanyindwa AMCOS uliamua kulipa shilingi milioni 10 kila msimu ili kupunguza deni hilo.