Waziri Bashungwa aipa NIDA miezi miwili vitambulisho viwafikie wananchi

0
32

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ametoa miezi kwa miwili Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhakikisha vitambulisho milioni moja na laki mbili ambavyo tayari vimeshatengenezwa vinasambazwa na kuwafikia wananchi walengwa.

Amesema hayo Jijini Dar es Salaam katika ziara ya kikazi ya kutembelea na kujionea utendaji wa Mamlaka hiyo ambapo ameiagiza NIDA kuhakikisha inatengeneza vitambulisho vipya bila gharama yoyote wala usumbufu kwa Watanzania ambao vitambulisho vyao vilifutika maandishi kutoka na tatizo lililotokea katika Uzalishaji.

“Niwajibu wenu kuhakikisha kadi hizi mnazifutilia na zinawafikia walengwa ndani ya miezi miwili kuanzia sasa, nitakapo rudi na kuomba taarifa ya kadi hizi zilizozalishwa nataka ziwe zimewafikia walengwa,” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameitaka NIDA kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi na kuondokana na tabia ya urasimu ambapo ameiagiza Menejimenti kuanza kuwachukuliwa hatua baadhi ya watumishi wazembe ambao hawatoi huduma nzuri kwa Watanzania.

Bashungwa amewakumbusha Watanzania kujenga utamaduni wa kujisajili ili kupata kitambulisho mara wanapotimiza miaka 18, na sio kusubiri mpaka kihitajike, ili kuondokana na usumbufu ambao mara nyingi hujitokeza wakati wa Usajili wa vyuo na kipindi cha vijana kujiunga na mafunzo mbalimbali.

Send this to a friend