Waziri Bashungwa ampa RC Makalla siku saba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla kukutana na LATRA, wadau na wamiliki wa mabasi kuweka uratibu mzuri wa kusimamia maelekezo ya Serikali kwa mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.
“Ninafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshapokea changamoto ya mabasi kutoingia ndani ya kituo hiki cha Magufuli na mimi nimekuta changamoto bado iko pale pale, sasa kwa sababu ameshanza kulifanyia kazi nampa siku saba awe amekutana na LATRA pamoja na wadu wa mabasi (TABOA) kuangalia utaratibu wa mabasi yote kuingia ndani ya kituo kushusha na kupakia abiria,” amesema Bashungwa.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 50 kujenga kituo hicho, hivyo Serikali haitakubaliana na watu ambao hawazingatii utaratibu uliowekwa katika kituo hicho.
Pja, ametoa siku 14 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, kamati ya fedha na uongozi wa kituo hicho kufanya mapitio na kupeleka mapendekezo ya changamoto ya wapangaji katika kituo hicho.
Hata hivyo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kheri James kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na wadau wa kituo hicho, mawakala na makarani ili kusikiliza na kuweka utaratibu wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika kituo hicho ili kuzitatua.