Waziri Bashungwa awaonya mashabiki wanaobeza timu zao

0
72

Waziri wa Utamaduni, Sana na Michezo, Innocent Bashungwa ameonya tabia ya mashabiki wa timu kubeza timu zao pindi zinaposhindwa kufikia malengo au hatua iliyotamaniwa na mashabiki husika akisema kitendo hicho siyo cha kizalendo na kinawavunja moyo wachezaji.

Bashungwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, katika kilele cha mashindano ya mpira wa miguu wa jimbo la Korogwe yaliyopewa jina la Dkt. Kimea Cup

Amesema Watanzania hawana budi kutambua kuwa michezo mingi humalizika kwa matokeo ya aina tatu, ambayo ni kufunga, kufungwa na kutoa sare, hivyo mashabiki hawana budi kuwa tayari kuyapokea matokeo yote matatu.

“Nyinyi nyote mnaoshindana leo ni wazuri ndiyo maana mmefikia fainali, hivyo nyote ni wangu lakini lazima mjue kwamba kwenye mchezo wa mpira wa miguu kuna kushinda, kushindwa na kupata sare, yote ni matokeo na yote lazima watanzania tuwe tayari kuyapokea,” amesema.

Mashindano ya Dkt. Kimea Cup yalishirikisha timu 12 kutoka kwenye kata 11 za Jimbo la Korogwe Mjini na kuziwezesha  timu ya kata ya Kwamndolwa na kata ya Mgombezi kuingia katika fainali ya mashindano hayo, mchezo uliochezwa katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Korogwe (Korogwe TCC)  Novemba 21, 2021.

Send this to a friend