
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema mtu aliyetajwa kwa jina la Mwijaku kwenye video za mgogoro wa mabinti wa vyuo atahojiwa kwa mujibu wa sheria, na baada ya hapo Wizara itachukua hatua zaidi.
Video hiyo iliyosambaa mitandaoni iliwaonesha mabinti kadhaa wa vyuo vikuu wakimfanyia udhalilishaji mwenzao, huku wakisikika kumgombania mtu aliyetajwa kwa jina la Mwijaku.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hawa naye atahojiwa kwa mujibu wa Sheria na baada ya hapo, Wizara yangu itaona nini ifanye kuhusu mustakabali mzima wa maadili ya jamii na nafasi ya huyo Mwijaku, na wengine wote wenye nafasi zenye kuchochea kasi ya athari chanya au hasi kwenye maadili ya jamii,” amesema Waziri.
Aidha, Dkt. Gwajima amewaomba wananchi wawe watulivu juu ya jambo hilo na kuendelea kufuatilia taarifa zitakazotolewa na Jeshi la Polisi ambalo linaendelea kuwahoji wahusika wa tukio hilo.