Waziri Jafo amuondoa Meneja wa TARURA kwa kutokusanya wananchi kushuhudia ukaguzi wa barabara

0
13

Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo amemuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) jijini Arusha, Podia Mwankenja kwa kushindwa kukusanya wananchi katika shughuli yake ya ukaguzi wa barabara za zilizokamilika kujengwa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari pamoja na viongozi mbalimbali mkoani Arusha Waziri Jafo amesema kuwa kitendo cha meneja huyo ambaye pia ndiye mratibu wa mradi wa barabara jiji humo ni hujuma zinazolenga kukwamisha jitihada za serikali kuwaonesha wananchi shughuli ilizofanya.

“Ina maana barabara hii ni ya kwenu, siyo ya wananchi? Kama ni barabara ya wananchi, mbona hawapo hapa? Au unataka ionekakana kama serikali haijafanya kitu kwenye eneo lao? Wewe ni mpinzani na wenzako? Maana yake nini,? amehoji waziri huyo akionesha kuchukizwa na kitendo cha wananchi kutokuwapo.

“Kwanini tunazindua barabara hii wananchi hawapo? Unataka Rais aonekane hajafanya kitu? Rais ameweka fedha hapa. Mmeficha watu wasijue halafu kesho na kesho kutwa mseme Rais hajafanya kitu?”

Kufuatia kitendo hicho, Waziri Jafo ameagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA apewe taarifa na mpangie Mwankenja kituo kingine cha kazi kwa sababu haiwezekani Rais Magufuli awekeze fedha nyingi za maendeleo halafu wao waseme kuwa hajafanya kitu.

Kwa upande wake Mwankenja akianza kujieleza kabla ya kukatishwa na waziri huyo amesema kuwa alipewa barua kuwa atashirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kujua ni barabara gani waziri atapelekwa.

“Mimi nimepewa barua kama copy (nakala) kwamba nitashirikiana na Mkurugenzi wa Jiji kwamba tutaangalia ni barabara gari waziri tutampeleka atembelee, sasa suala la kwamba wananchi,” alinyamaza kiongozi huyo baada ya kukatishwa wakati akijieleza.

“Ninyi ndio wataalamu mnaofanga Serikali ionekane haijafanya jambo wakati sisi hapa Arusha tumewekeza fedha nyingi. Mji wa Arusha tumetandaza barabara ila wewe unaficha hata wananchi hapa jirani wasijue tumeweka barabara,” amehitimisha Waziri Jafo akisisitiza kuwa hapendi uzembe katika kazi.

Send this to a friend