Waziri Kombo akazia matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa nchi za Jumuiya ya Madola

0
45

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amezitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kama moja ya mbinu za kufikia mpango wa Jumuiya hiyo wa kuzalisha nishati endelevu.

Waziri Kombo ameyasema hayo wakati wa majadiliano ya Ajenda ya Jumuiya ya Madola ya Nishati Endelevu ‘The Commonwealth Sustainable Energy Transitions Agenda (CSETA)’ yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaoendelea Apia, Samoa.

Katika maelezo yake, Waziri Kombo ameeleza changamoto pamoja na fursa zinazopatikana nchini katika uwekezaji wa mpango wa nishati safi na endelevu, akigusia kuwa changamoto kubwa ni gharama kubwa za huduma za nishati safi ya kupikia, suala la tamaduni na mazoea ya watu kutumia kuni au mkaa kupikia na hivyo kuchelewesha Tanzania kufikia mabadiliko yanayokusudiwa kwa haraka.

Aidha, Waziri Kombo ameelezea namna Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kupigia debe ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na kutoa kipaumbele cha ajenda hiyo kwa wanawake ambao wanaathirika zaidi kiafya kutokana na moshi wa kuni za kupikia au mkaa na kuialika Jumuiya ya Madola kutumia fursa za ushirikiano kwenye nishati pamoja na uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Dkt. Arjoon Suddhoo amesema mjadala huo utasaidia Jumuiya ya Madola kuona ni kwa namna gani inaweza kushirikiana vyema zaidi katika kukuza matumizi ya nishati endelevu hasa katika kujenga uwezo na kubadilishana teknolojia ili kuharakisha kufikia Ajenda ya Nishati endelevu kwa wote hadi kufikia mwaka 2030.