Waziri Kombo amwakilisha Rais Samia CHOGM

0
36

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 49 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaoendelea Apia, Samoa kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024.

Kati ya mambo muhimu katika mkutano huo ni pamoja na kumchagua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Masuala mengine nyeti yatakayojadiliwa ni pamoja na uwekezaji, kutafuta suluhu ya pamoja kwa ajili ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, uchumi, demokrasia, na amani.

Mkutano huu utaibua changamoto na matarajio ya wanachama, huku Tanzania kama moja ya wanachama 56 wa Jumuiya ya Madola ikiwa miongoni mwa wale watakaonufaika katika sekta za uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi, uchumi stahimilivu, na kubadilishana ujuzi kati ya mafanikio mengine mengi.

Waziri Kombo amewasili Samoa na kupokelewa na Waziri wa Fedha wa Samoa, Lautimuia Vaʻai ambapo akiwa safarini, Kombo amefanikiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Utalii wa Seychelles, Sylvestre Radegonde.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ya kimaendeleo ‘One Resilient Common Future: Transforming Our Common Wealth.’

Send this to a friend