Shilingi bilioni 10 kupambana na tatizo la Watanzania 33,000 kufariki kila mwaka kwa kutumia nishati isiyo safi kupikia

0
37

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 10 kusambaza gesi majumbani na viwandani ili kupambana na athari zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo salama majumbani.

Amesema hayo leo Oktoba 12, 2022 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ambapo amesema zaidi ya Watanzania 33,000 hufariki kila mwaka kutokana kupumua moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Ameongeza kuwa uchambuzi wa matumizi ya nishati nchini unaonyesha 8% pekee ya Watanzania hutumia nishati safi ya kupikia isiyotoa moshi unaoangamiza afya zao, huku asilimia 70 ya magonjwa nchini yakiwa ni magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Ili kupambana na hayo, Waziri Makamba amesema Serikali imeandaa mjadala wa kitaifa utakaoleta suluhu ya namna ya upikaji kwa Watanzania ambao utawezesha kuweka mifumo ya kisera, mifumo ya kisheria, kikodi  na kiutawala ili kuondokana na matumizi yasiyo salama.

Kongamano hilo litakuwa na madhumuni matano ambayo ni kufahamu hali ya sasa ilivyo ya nishati ya kupikia na upikaji, kubadilishana uzoefu, ujuzi na fursa zitakazoweza kuondokana na kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kupitia na kujadili sera, sheria pamoja na mikakati ya kifedha na kiteknolojia itakayowezesha kuelekea kwenye nishati safi na salama, kutafuta namna bora ya kufikia malengo hayo na kutengeneza ushirikiano, maelewano na mwendo wa pamoja miongoni mwa wadau.

Send this to a friend