Waziri Mbarawa: Wakati ajali ya ndege inatokea, boti ya uokoaji ilikuwa mbali

0
22

Serikali imesema wakati wa ajali ya ndege ya Precision Air boti ya uokozi ilikuwa katika doria kwenye maeneo ambayo ni mbali na ulipo uwanja wa ndege wa Bukoba ikiwa katika kutekeleza majukumu ya kawaida ya doria.

Ameyasema hayo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwasilisha taarifa ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya kampuni ya Precision Air iliyopata ajali Novemba 6 mwaka huu Bukoba, mkoani Kagera.

“Natambua kuwa uwezo wa kukabiliana na ajali na majanga unahitaji kuboreshwa zaidi, na naomba kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wanaohusika katika masuala ya uokozi katika kuimarisha uwezo wetu,” amesema.

Aidha, amefafanua kuwa kiwanja cha ndege cha Bukoba kina kituo cha zimamoto ambacho kina gari la kuzima moto na kikosi cha wafanyakazi kumi (10) wenye jukumu la kutoa huduma za uokoaji katika matukio ya ardhini.

Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa ajali hiyo haikutarajiwa, na kwamba ajali inapotokea huambatana na madhara ambayo kila mtu ana wajibu wa kushiriki kukabiliana nayo.

“Ajali ilipotokea wadau mbalimbali walijitokeza kushiriki kuokoa kama ambavyo hufanya katika ajali zingine zote, na Serikali imefanya juhudi zote zilizowezekana kukabiliana na madhara ya ajali hii,” amesema Mbarawa

Send this to a friend