Waziri Mkenda afafanua utaratibu wa ufanyaji mitihani kwa walimu

0
23

Serikali imesema walimu wapya ndio watakaohusika na utaratibu wa kufanya mitihani kabla ya kuajiriwa ambapo utekelezaji wa utaratibu huo utafanyika baada ya sera hiyo kupitishwa ili kuwapata walimu wenye ubora.

Waziri wa Elimu, Adolf Mkenda amesema walimu walio tayari kazini hawatahusika na ufanyaji mitihani, bali watasaidiwa kwa kufanyiwa semina na mafunzo pamoja na kutoa fursa mbalimbali za masomo ili kujiendeleza.

“Suala la msingi hapa ni kwamba ni walimu wapya ndio ambao tutakuwa na utaratibu wa kuwachuja kwa kupitia mitihani, na hiyo ipo kwa madaktari, kwa fani nyingine za sheria n.k. Sasa hawa madaktari na wanasheria wote wanapitia mikononi mwa walimu, kwahiyo walimu ni muhimu sana kwa sababu ndio wanaotufundishia madaktari wetu baadaye, wanasheria nk,” amesema Mkenda.

Aidha, Waziri Mkenda amefafanua kuwa mbali na lengo la Serikali kupata walimu walio bora kupitia ufanyaji wa mitihani, pia ina lengo la kurudisha hadhi ya ualimu ambayo imekuwa ikichukuliwa kama kazi ya kawaida.

“Sera hiyo itapitishwa baada ya kupitia Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Kamati ya Makatibu wakuu na kisha kwa Baraza la Mawaziri ambao watamshauri Rais kuridhia ama la,” amesema Prof. Mkenda.

Send this to a friend