Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa ruhusa ya waliokatisha masomo kwa ujauzito kurejea shule haimaanishi kwamba wanaruhusiwa kwenda na watoto darasani.
Agizo hilo la Mkenda limekuja siku chache baada ya kuonekana kwa picha za msichana aliyekatisha masomo kwa kupata ujauzito akiwa amerejea darasani na mwanae wa miezi minne.
Mkenda amesema hali hiyo hairuhusiwi kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuwasumbua wanafunzi wengine wakiwa darasani.
Msichana arejea shule na mwanae wa miezi minne
Mwanafunzi huyo, Esnath Gedion kutoka mkoani Mbeya amekuwa akiingia darasani na mwanae mwenye umri wa miezi minne, baada ya kukosa mtu wa kukaa na mtoto wake nyumbani.
Baadhi ya wadau wa elimu, wanasema, serikali ilitakiwa kuweka miundombinu rafiki kwanza kwa wanafunzi hao na watoto wao.
Mbali na waliorejea katika mfumo rasmi wa elimu, wanafunzi wengine wamerudi shuleni kupitia mradi wa Alternative Education Pathway, ambao ni wezeshi na hauna masharti magumu kwa wanafunzi kama vile kuvaa sare darasani.