Waziri Mkuu aagiza mkandarasi akamatwe na azuiwe hati ya kusafiria

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amelielekeza Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuhakikisha wanamkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala mkoani Singida.
Amesema mkandarasi huyo aliaminiwa na Serikali kwa kupewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2016. Mradi huo ulipaswa kukamilika mwaka 2018.
Akitoa agizo hilo wakati akikagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida, amesema jitihada zimefanyika za kuona mradi huo unaendelea lakini mkandarasi amekuwa akileta ugumu katika utekelezaji. “Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwa sababu ameicheleweshea mradi.”
“Naelekeza, Kamishna wa Uhamiaji, kamata hati yake ya kusafiria, asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe, hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi anaifanyia nchi yetu, Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemuajiri, tunamlipa lakini anajiamulia kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Ameongeza kuwa wakandarasi wa nje wanapaswa kufahamu kuwa wanapokuja nchini kufanya kazi watambue Tanzania imewaajiri na hivyo wasijione kama wao ni mabosi.








