Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusitisha mara moja utaratibu wa kikosi kazi (Task Force) kwenye makusanyo ya kodi kwa wafanyabiashara kwani huchangia kamata kamata na rushwa.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kufuatia mgomo ulioanzishwa Mei 15, 2023 wakidai kuwepo kwa urasimu bandarini, kamata kamata zilizokithiri pamoja na malalamiko ya sheria mpya ya usajili wa stoo.
“Task force hii ndio inaendesha kamata kamata kila siku, Kamishna wa Mapato ya Ndani TRA naagiza isitishwe, kanuni zipo sheria zipo zinatuelekeza namna ya kulipa kodi, kamata kamata hii inafukuza wafanyabiashara Kariakoo na mbaya zaidi mnawakamata hadi wageni kutoka nje,” amesema Waziri Mkuu.
TRA: Ukamataji unafanyika tunapofanya ukaguzi kujiridhisha
Aidha, amewasihi wafanyabiashara kusitisha mgomo huo akiahidi kutatua kero zao pamoja na kuepuka kuwapoteza wateja kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi na kuendelea kulinda hadhi ya soko hilo kimataifa.
Naye, Mbunge wa jimbo la Ilala ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu ameahidi kuwashughulikia watumishi wa TRA waliokaidi maagizo ya Rais Samia Suluhu wakisema “ni maagizo ya kisiasa tu,” akidai kitendo hicho ni kudharau mamlaka ya Rais.