
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewahimiza wananchi wa Itilima mkoani Simiyu kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Itilima wilayani Itilima mkoani Simiyu leo, Waziri Mkuu amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kueleza mafanikio yaliyopatikana kupitia Serikali ya CCM ili wagombea wa chama hicho wasipate kazi kubwa katika kampeni.
“Mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu, vyama vyote vitakuja kuomba kura, lakini nyinyi mnajua kuwa CCM inapeleka wagombea wake katika nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani. Kwa nafasi ya Urais, mgombea wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwa Zanzibar ni Dkt. Hussein Mwinyi, huku mgombea mwenza akiwa ni Balozi Dkt. Nchimbi. Watazunguka nchi nzima kuomba ridhaa ya Watanzania,” amesema Waziri Mkuu.
“Mpango wetu kwa Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kwamba wagombea wetu watakapopita kwenye maeneo yetu wasipate kazi kubwa ya kueleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo husika, kazi hiyo itafanywa na wana-CCM mlioko kwenye eneo hilo,” ameeleza.
Aidha, Majaliwa amesema wilaya hiyo tayari ina zahanati 37, na lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati yake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.