Waziri Mkuu asisitiza Uchaguzi Mkuu kufanyika Oktoba kama ilivyopangwa

0
93

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 yanaendelea kama yalivyopangwa, huku akiwataka wananchi na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika mchakato huo muhimu wa kidemokrasia.

Akizungumza leo wakati akitoa hotuba ya kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi huo, na kwamba Serikali itahakikisha kila raia mwenye sifa anapata haki ya kupiga kura au kugombea bila vikwazo.

“Nitumie fursa hii kuwakumbusha wadau mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake, ikiwemo wananchi ambao ni wapiga kura, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo,” amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa amani na utulivu wa nchi ni tunu ya kipekee ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda kwa nguvu zote kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha analinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu wa nchi yetu. Kwa upande mwingine, Serikali itatekeleza wajibu wake wa kusimamia Katiba, sheria na taratibu zilizowekwa ili kila mwananchi mwenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa aweze kutimiza haki yake ya kikatiba bila vikwazo vya aina yoyote,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Send this to a friend