Waziri Mkuu awaondoa watumishi 16 MSD

0
44

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Mei 9 amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua.

Akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vya kutengeneza barakoa na dawa vilivyopo katika eneo la MSD, Keko jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amesema kuwa MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa bila ya mikataba halali jambo ambalo si sahihi.

Aidha Waziri amesema kuwa taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.52 kwa wazabuni sita bila ya kufuata utaratibu na wala kuitaarifu bodi ya zabuni ya MSD.

Pia zabuni 23 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.55 zilifanywa nje ya Mfumo wa Ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na PPRA kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi.

Amesema taasisi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi milioni 215 kwa ajili ya kugharamia posho ya watumishi watatu waliokwenda China kwenye majadiliano ya kuleta mashine za dialysis kwa siku 61.

“Watumishi watatu wameenda China kufanya majadiliano, kwa nini wasimtumie Balozi wa Tanzania nchini China kufanya shughuli hiyo. Si utaratibu kukaa siku 61 kwa ajili ya majadiliano tena bila ya kuhusisha menejimenti ya taasisi,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema katika taasisi hiyo kuna udhahifu wa usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi licha ya kuwa wamelipwa, na katika idara ya manunuzi kumebainika kuwepo kwa watumishi ambao si wataalamu, hivyo ameagiza wote 16 waondolewe.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata dawa.

Send this to a friend