Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awataka Watanzania kuiamini serikali vita ya corona

0
44

Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa, waziri mkuu amewasihi Watanzania kuiamini serikali pamoja na watalamu wa afya katika mapambano dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Majaliwa ameyasema hayo katika maombi maalum ya kitaifa yaliyoandaliwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ambayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.

“Nina fahamu baadhi ya Watanzania wenzetu wangependa kuona hatua zaidi zinachukuliwa kukabiliana na virusi vya corona, lakini ni muhimu waelewe kuwa kila hatua ina faida na hasara zake. Hivyo, serikali inaendelea kupitia kila hatua ione manufaa na hasara zake,” amesema Majaliwa.

Baadhi ya watu wamekuwa wakiishinikiza serikali kuchukua hatua kali kukabiliana na virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kulifunga (lockdown) Jiji la Dar es Salaam na kuzuia mikusanyiko ya kidini.

Hivi karibuni akizungumzia hatua ambazo serikali imechukua kukabiliana na COVID-19, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa sio kila hatua iliyochukuliwa na nchi za magharibi itaafaa kutumika Tanzania, na kwamba ‘lockdown’ itaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi ambapo kipato chao ni kwa siku.

Hadi Aprili 21 mwaka huu Tanzania ilikuwa na visa 284 ambavyo ni pamoja na vifo 10 na watu 11 waliopona.

Send this to a friend