Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali haijazuia watu kwenda kwenye nyumba za ibada kusalia, ili waumini watumie ibada hizo kuliombea taifa.
Waziri mkuu amesema hilo alipokuwa akizungumza na viongozi wa mikoa kuhusu utaratibu wa mikusanyiko katika makanisa na misikiti ikiwa ni mkakati wa kudhibiti virusi vya corona ambapo ameeleza kuwa, licha ya serikali kuruhusu ibada za Ijumaa na Jumapili kufanyika, lakini ni lazima tahadhari zichukuliwe kuhakikisha waumini wanakuwa salama.
“Tulichoacha ni ibada. Ili ibada hizo zisaidie waumini kuliombea taifa hili. Tena tumesisitiza katika kanisa hilo, katika msikiti huo, lazima wajali kukaa kwa nafasi. Tumesema watu waende kwenye ibada, na ikiwezekana wachaguliwe wachache wa kwenda,” amefafanua waziri mkuu.
#COVIDー19
— Swahili Times (@swahilitimes) April 16, 2020
Serikali imezuia shule za Jumapili za watoto (Sunday Schools) makanisani, pamoja na Madrasa misikitini kwa maelezo kuwa mikusanyiko hiyo imezuiwa, na kwamba kilichoruhusiwa ni ibada za Ijumaa na Jumapili, tena zinazopaswa kuwa fupi iwezekanavyo. pic.twitter.com/HWmQuLONiE
Aidha, amesema kuwa licha ya serikali kuruhusu ibada hizo ambazo zinatakiwa kufanyika kwa muda mfupi, lakini shule za watoto za jumapili (sunday schools) pamoja na madrasa haviruhusiwi.
Ameongeza kuwa serikali inatambua kwamba bado kuna masoko, maduka na supermarkets ambazo walisema watu waendelee kupata huduma , na kwamba serikali haikusudii kusitisha watu kupata huduma kwenye maeneo hayo.
Hata hivyo ameyaagiza maduka yote kuweka ndoo za maji na sabuni kwenye milango, ili mteja anapokuja anawe, ili hata anapokamata bidhaa na kuiacha, basi ibaki kuwa salama.