Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Afrika wa Zana Endelevu za Kilimo (Africa Sustainable Agricultural Mechanization) utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026, sambamba na uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo muhimu kwa mustakabali wa kilimo barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Albert Chalamila, amesema mkutano huo unafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Ameeleza kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa nchi za Afrika kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kuharakisha matumizi ya zana na teknolojia za kisasa za kilimo kwa ajili ya mageuzi endelevu ya sekta hiyo.
Chalamila ameongeza kuwa kupitia mkutano huo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuzindua rasmi Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili, ambao utakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa. Mkutano huo pia unatarajiwa kuhudhuriwa na Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wadau wa sekta hiyo.
Amesema tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha sekta ya kilimo kwa masilahi mapana ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la FAO nchini, Charles Tulai, amesema mkutano huo ni muhimu katika kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu. Ameeleza kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake katika kuendeleza kilimo barani Afrika.
Tulai ameongeza kuwa vijana wanatajwa kuwa nguvu kazi muhimu katika mageuzi ya kilimo, na mkutano huo utakuwa jukwaa la kuhimiza ushiriki wao katika matumizi ya teknolojia na zana za kisasa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na ajira katika sekta ya kilimo.








