Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya kurekodi matukio ya kuzua taharuki na kuyarusha kwenye mitandao ya kijamii badala yake wanapaswa kuripoti taarifa hizo kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe.
Ameyasema hayo bungeni jijijni Dodoma wakati akitoa ufafanuzi na mwelekeo wa Serikali kuhusu changamoto ya nidhamu na malezi ya wanafunzi pamoja na adhabu zinazotolewa na walimu shuleni, ambapo amesema lengo la kutosambaza matukio hayo sio kuficha taarifa bali ni kuzuia taharuki, chuki na uhasama ndani ya jamii.
“Nitoe wito kwa jamii hasa wale wanaochukua au kupata matukio na kuyarusha kwenye mitandao kutofanya hivyo kwani yanajenga chuki kwa walimu [..] Pale matukio kama haya yanapojitokeza utaratibu umewekwa, taarifa zake zitumwe kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe huko huko kuliko kuleta taharuki kwa jamii nzima,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, amesema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa walimu pamoja na walimu wakuu ambao watakiuka utaratibu wa adhabu uliowekwa, kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji wa nidhamu shuleni chini ya kifungu namba 61 cha sheria ya elimu, sura ya 353 na kanuni zake.
Ufafanuzi wa Serikali kuhusu kutotangaza shule bora kidato cha nne
Waziri Mkuu ametoa wito kwa walimu wakuu na wakuu wa shule kutumia walimu wa malezi, ushahuri na unasihi pamoja na viongozi wa dini walioko jirani katika kuwarekebisha watoto na kuwajenga kimaadili ili kuepuka adhabu za viboko pale ambapo si lazima kutumika.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia weledi, kanuni na uadilifu kwenye utumishi katika nyanja zote na katika kila sekta, na kwamba endapo patajitokeza uvunjifu wa maadili hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa.