Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina lengo la kuwawezesha na kuwasimamia wafanyabiashara kufanya shughuli zao pamoja na kutekeleza vyema majukumu yao ili kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Amesema hayo wakati wa kikao na wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Kariakoo kilichofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam ambacho kilikuwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zao.
“Dhamira ya dhati ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya biashara ili kila Mtanzania anayeamua kufanya biashara aweze kupata tija, ni dhamira ya wazi na ina maelekezo kwetu wasaidizi, tuyafanyie kazi na tuyasimamie, tutoe mrejesho wa mafanikio,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amekemea tabia ya watumishi hususani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha tabia ya kuwaomba wafanyabiashara barua ya Rais Samia kama uthibitisho wa maagizo aliyokwishatoa.
Serikali yaunda tume kushughulikia changamoto za wafanyabiashara
“Mamlaka ya mapato nisisikie tena mkiomba barua ya Rais kwa wafanyabiashara ndipo ufanye kazi yako, kwani anapozungumza hamkai kwenye TV? Hamkai kwenye radio?” amehoji.
Kuhusu suala la kukutana na Rais Samia, Waziri Mkuu amesema Rais ni taasisi kubwa na mwenye mambo mengi ya kitaifa na kimataifa, hivyo ni wajibu wa wasidizi wake kuwasikiliza na kutatua matatizo yao kwa niaba yake.