
Kassim Majaliwa leo Machi 13, 2025 amezindua kituo kipya cha mabasi cha Nzega mjini ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 4.327.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa kituo hicho ambacho utekelezaji wake umefikia asilimia 100, Waziri Mkuu ameipongeza halmashauri hiyo kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo hicho kwani kitaibua fursa za biashara kwa wakazi wa eneo hilo.
“Tunataka wananchi wengi zaidi wanufaike, ongezeni vibanda, huu ni ubunifu mzuri sana utasababisha wengi wanufaike, waleteni wajasiriamali hapa wapate rizki zao, mkifanya hivyo mtaongeza mzunguko wa fedha,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na mpango kazi wake wa kuwahudumia watanzania wakati wote, “Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kukamilisha malengo yake katika kuwatumikia watanzania.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kujielekeza katika kutatua changamoto za wananchi kupitia mapato yao ya ndani kutekeleza miradi.