Waziri Mkuu: Serikali inathamini mchango wa viongozi wa dini

0
7

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa waumini wa madhehebu mbalimbali nchini kuzingatia sheri ya uhuru wa kuabudu ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Ameyasema hayo katika Swala na Baraza la Eid Al Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Mohamed VI Kinondoni, Dar es Salaam ambapo amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuwajenga waumini wao kuwa na staha, ustaarabu, uvumilivu na kutambua kuwa wao ni miongoni mwa wanajamii na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.

“Tunaamini mtaendeleza jukumu la kuwasihi watanzania waone umuhimu wa kila mmoja kuwa sehemu ya mchango wa kulifanya taifa hili kuwa tulivu na kuimarisha mshikamano miongoni mwetu.” amesema Majaliwa.

Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inawaamini na inathamini mchango wa viongozi wa dini wa madhehebu yote na kwamba itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na viongozi hao ili kujenga amani, mshikamano na ustawi wa jamii ya watanzania.

“Kwa upande wa serikali tunaendelea kujenga misingi ya mshikamano kati ya waumini wa dhehebu moja na dhehebu jingine, tukiwa tunaamini kuwa dini zimeendelea kuifanya nchi hii kuwa nchi ya amani wakati wote,” amesema.

Aidha, amewasihi watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa hususan Rais Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe nguvu na afya ya kuendelea kuliongoza taifa.