Viwanda vipya zaidi ya 4,000 vilivyojengwa katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania kuanzia mwaka 2015 vimetoa maelfu ya ajira kwa wananchi ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja.
Akitoa takwimu hizo bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.
“Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi nzima,” amesema kiongozi huyo.
Aidha, ameongeza kuwa katika mwaka 2020/2021, serikali itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda, ambapo lengo ni kuimarisha msingi wa ukuaji wa sekta ya viwanda nchini pamoja na kuvutia sekta binafsi kuwekeza au kushirikiana na Serikali kuwekeza kwenye viwanda.