Waziri Mwambe: Hakuna uhaba wa mafuta ya kula nchini

0
13

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe amewaonya wafanyabiashara wa mafuta watakao pandisha bei ya bidhaa hiyo kinyume na bei elekeze kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao za biashara.

Waziri Mwambe ametoa onyo hilo leo Januari 26, 2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari juu ya mfumuko wa bei ya mafuta ambao umekua mkubwa kwa siku za hivi karibuni.

Amesema hakuna uhaba wa mafuta nchini, badala yake mafuta hayo yamekuwa yakiuzwa bei ghali. Amesema tayari meli moja imeshashu mafuta nchini, na nyingine moja itashusha hivi karibuni ambapo jumla ya mafuta hayo ni takribani tani 48,000 huku mahitaji ya mwezi yakiwa tani 30,000.

“Kwa sasa changamoto ya bei haitakuwepo na tayari tumeshawapunguzia waagizaji baadhi ya gharama za kushusha mafuta pale bandarini lakini pia niwahakikishie watanzania uhaba wa mafuta hauwezi kuendelea kwani Februari 17 kuna meli ya mafuta itawasili na nimeagiza isichukue muda mrefu kushusha pale bandarini hadi Februari 20 meli hiyo iwe imeshashusha mafuta,” amesema.

Aidha, ametoa maelekezo kwa Tume ya Ushindani kuhakikisha wanafuatilia mwenendo wa mafuta nchini huku akiwataka kumuandalia ripoti ya hali ya bidhaa hiyo hapa nchini nchini.

Amewataka Wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao ina ardhi inayokubali mazao ya mafuta kama michikichi, alizeti na karanga na mazao mengine ya mafuta kuhamasisha Wananchi wao kujikita kwenye kilimo hicho ili kuweza kujikwamua kiuchumi wao wenyewe lakini pia kuzalisha mbegu ambazo zitatumika na viwanda vya ndani na kupunguza uagizwaji wa mafuta nje ya nchi.

Send this to a friend