Waziri Nape azindua ofisi ya kisasa ya Vodacom jijini Dodoma

0
60

Waziri Mkuu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye amepongeza jitihada za Vodacom Tanzania kwa kufungua ofisi ya kisasa katika makao makuu ya nchi, Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali kuhamishia sehemu ya shughuli zake jijini humo pamoja na kusambaza huduma za mawasiliano na kiteknolojia nchini kote.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo leo mpya ya kisasa makao makuu ya nchini mkoani Dodoma, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia na Habari, Mh. Nape Nnauye amepongeza jitihada hizo zikiwa zinalenga kuwasogezea Watanzania huduma bora na za uhakika popote walipo kama serikali inavyofanya kuhamishia baadhi ya shughuli zake katika makao makuu ya nchi ili kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu mpaka Dar es Salaam.

“Kwa kipindi kifupi sekta yetu imeshuhudia mafanikio makubwa yakujivunia ambayo ni mchango mkubwa katika maendeleo yetu. Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya watumiaji wa simu kutoka laini zilizosajiliwa Milioni 51.3 mwaka 2020 hadi kufikia watumiaji Milioni 61.88 mwezi machi, 2023 ambapo kati ya hao asilimia 30 wanamilikiwa na vodacom. Katika kipindi hicho hicho watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka watumiaji Milioni 26 hadi milioni 33.1. Fanikio lingine ni kwa upande wa ‘financial inclusion’ ambapo kwa sasa watumiaji wa huduma za “mobile money” hapa nchini wameongezeka hadi kufikia wateja milioni 44.4 ambapo kati yahao asilimia 36 wanamilikiwa na Vodacom kupitia M-PESA,” alisema Mh. Nnauye.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye (katikati) akizungumza na viongozi wa Vodacom Tanzania wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya yenye ubora na uwezo sawa na ya makao makuu ya Dar es Salaam ikiwemo kuhudumia wasioona na kusikia pamoja na chumba maalum cha wajawazito na waliojifungua, makao makuu ya nchi, jijini Dodoma leo. Wakimsiliza kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mh. Selemani Kakoso wakati kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Linda Riwa, Mkuu wa Kanda ya Kati, Joseph Sayi, na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire (kwa nyuma).

Mnamo mwezi Mei 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa makampuni yote ya mawasiliano kupanua wigo wa huduma zao kwa kuzipeleka maeneo ya vijijini ambapo ndipo kuna Watanzania wengi zaidi.

Katika hafla hiyo ya utiaji Saini ya kusambaza huduma za mawasiliano kwa kata 713 ambapo minara takribani 758 inatarajiwa kujengwa, serikali iliweka wazi nia yake ya kutaka kuwafikishia huduma za mawasiliano Watanzania kwa asilimia 80 ifikapo 2025 ambapo watoa huduma ni wadau muhimu.

Pia, Waziri Nnauye amewapongeza Vodacom kwa uwekezaji, katika kupanua wigo wa mtandao wao, kuboresha ubora wa huduma, kuanzisha teknolojia mpya na uvumbuzi, mfano mzuri ni huduma ya M-Mama, inaendelea kuboresha maisha ya watanzania na kuchangia ukuaji na maendeleo ya sekta. Pamoja na upatikanaji wa huduma ya 5G jijini Dodoma inayopatikana kwa kupitia minara 5 na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye mtandao wa 5G.

“Ningependa kuihakikishia sekta binafsi nchini kuwa Dodoma ni jiji linalokuwa kwa kasi ukiachana na kuwa ni makao makuu ya nchi, lakini pia ni eneo ambalo limekaa kimkakati kwa shughuli za kibiashara. Nimefurahishwa pia kuona duka lenu lina dawati la watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa sawa ya kupata huduma zenu. Tunaposema ujumuishwaji wa kidijitali, ni pamoja na kuhakikisha kuwa watu wote wana uelewa na ujuzi wa kutumia huduma hizi za kidijitali,” alimalizia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire amesema kuwa ni furaha hatimaye kufungua ofisi mpya ya kisasa katika makao ya nchi, Dodoma, kuwahudumia wateja na wageni mbalimbali wa ndani na kimataifa wanaofika kwa shughuli binafsi na za kiserikali.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania, Joseph Sayi (kushoto), wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya ya kampuni hiyo yenye ubora na uwezo sawa na ya makao makuu ya Dar es Salaam ikiwemo kuhudumia wasioona na kusikia pamoja na chumba maalum cha wajawazito na waliojifungua, makao makuu ya nchi, jijini Dodoma leo. Akimfuatia kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mh. Selemani Kakoso Pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo.

“Ni furaha kuzindua ofisi mpya na ya kisasa ambayo ina sifa sawa na ya makao makuu yetu ya Dar es Salaam. Ofisi hii kubwa na bora inajumuisha chumba cha Mkurugenzi Mtendaji pamoja na vya mikutano kwa ajili ya shughuli tofauti. Pia, tumezingatia suala la usawa na ujumuishi kwa wateja wetu wote hususani walemavu. Ofisi hii ina uwezo wa kuwahudumia wasiosikia au viziwi kwa alama za vidole na kutokuona au vipofu kupitia ‘SAUTI PASS’ inayomwezesha kutumia sauti yake kupata huduma. Lengo kubwa ni kuwajali wateja wetu na kuwapatia fursa ya kufurahia mawasiliano na kujiunga kidigitali. hii ni kuendana na dhamira yetu ya kuwa wabunifu kwa kuwapatia ufumbuzi katika kuwasiliana na kuzifikia huduma zetu,” alisema Bw. Besiimire.

Bw. Besiimire alimalizia kuwa, “ofisi hii mpya pia itakuwa na chumba mahususi kwa ajili ya wajawazito na kingine kwa ajili ya michezo mbalimbali. Kwa kuongezea, kujali ustawi wa wafanyakazi wetu tutakuwa na chumba maalum cha utulivu, ‘the Quiet Room’. Hii tumezingatia kuwapatia fursa wafanyakazi wakiwa kwenye hali tofauti kufanya kazi zao kwa ufanisi kuendana na mazingira. Dhamira ya Vodacom siku zote ni kuwaunganisha Watanzania na huduma bora na uhakika za mawasiliano na teknolojia kwa kuzingatia ubunifu wa kidigitali. Niwasihi wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani kuitumia ipasavyo kuanzia leo kwani itakuwa inafanya kazi ipasavyo kwa huduma na bidhaa tofauti tunazozitoa nchini kote.”

Send this to a friend