Waziri Ndugulile atoa siku saba hoja za CAG zijibiwe

0
51

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameziagiza taasisi zilizo chini ya wizara yake kutoa majibu ya hoja za ripoti ya CAG ndani ya siku saba kuanzia Aprili 20, 2021.

Dkt. Ndugulile amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao chake cha kazi cha wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo cha kujadili na kufanya mapitio ya taarifa za mapato na matumizi za taasisi hizo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Amezielekeza taasisi hizo kutolea ufafanuzi maeneo ambayo yaliguswa katika taarifa ya CAG na kama kuna hoja zozote ziliyojitokeza zijibiwe kikamilifu na kuwasilishwa ndani ya wiki ijayo.

Aidha, ameziagiza taasisi ambazo hazikuwasilisha hesabu zao kwa CAG zitoe maelezo kwa nini hazikuwasilisha kwa mujibu wa taratibu za Serikali.

Katika hatua nyingine ameiagiza TCRA na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma kwani ikitolewa kwa kiwango kinachojitosheleza itapunguza baadhi ya malalamiko ya wananchi.

“Kuna mambo ambayo ni muhimu wananchi kuyafahamu kwa mfano matumizi makubwa ya data yanayosababishwa na settings za simu janja ambazo zinaruhusu baadhi ya programu kujiboresha zenyewe nazo zinachangia vifurushi vya data kuisha haraka.” amezungumza Dkt. Ndugulile

Send this to a friend